CCM NA CHADEMA WAKUNJANA MASHATI KINONDONI
TAFRANI: ZIARA YA WAZIRI Wanachama wa CCM na Chadema wakizozana katika eneo la Mavurunza, Dar es Salaam jana wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla kukagua miradi mbalimbali ya maji kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani
Ziara ya Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla jana iliingia dosari baada ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Salum Madenge na Diwani wa Kata ya Kimara, Paschal Manota (Chadema), kurushiana matusi .
Tukio hilo lilitokea jana wakati wa mkutano wa wananchi wa Kata ya Saranga, Kimara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Mavurunza ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya Makalla katika ukaguzi wa miradi maji ya Dawasco.
Vurugu hizo zilitokea baada ya Makalla kuagiza polisi kuwakamata wafuasi wa Chadema kwa madai kuwa walitaka kuvuruga mkutano huo. Baada ya Makalla kutoa agizo hilo, Diwani Manota na Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika walisimama na kupinga uamuzi huo na walirushiana maneno na Mwenyekiti Madenge aliyesema wawili hao waache upumbavu.
“Unatetea nini? Acha upumbavu... Hatuwezi kuendesha mkutano na watu wanaofanya vurugu,” alitusi Madenge huku Manota akiwa na jazba kabla ya viongozi wengine wa kisiasa kuwatuliza.
Hata hivyo, kabla ya Makala kuzungumza, Mnyika aliyekuwa ameongozana naye katika ziara hiyo alikuwa na wakati mgumu wa kuzungumza kutokana na zomeazomea kutoka kwa wafuasi wa CCM.
Makalla alisema kosa kubwa lililosababisha kutokea kwa vurugu hizo ni maandalizi mabovu ya wafuasi wa vyama vyote.
“Wafuasi walikuwa na itikadi zao zaidi kuliko kuja kusikiliza hoja za serikali kupitia ziara. Pia labda waliwakosa uvumilivu kutokana na ahadi ya maji kuwapo kwa muda mrefu, lakini kuvurugana wanasiasa ni kukosa uvumilivu,” alisema.
Kwa upande wake, Mnyika alipendekeza ziara zote za kiserikali zisiwe na uhusiano na vyama vya kisiasa.
“Kama ingekuwa ni mambo ya kuzungumzia ilani ya chama, tangu mwaka 2005/10 ahadi ya maji ya asilimia 90 kwa Jiji la Dar es Salaam haijatekelezwa,” alisema Mnyika.
No comments