MATOKEO YA KIDATO CHA SITA YA MWAKA 2014 YAWEKA HISTORIA
Matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka 2014 yaliyotangazwa juzi na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), yamewaacha wananchi wengi wakiwa midomo wazi.
Matokeo hayo yameacha historia katika nchi yetu, ikiwa ni rekodi ambayo tunalazimika kuiona kama muujiza wa karne, ingawa hatuoni uwezekano wa hali hiyo kujirudia katika miaka mingi ijayo kwa kuwa siyo tukio la kawaida.
Matokeo ya mtihani huo uliofanyika Mei mwaka huu yameonyesha kwamba watahiniwa 38,905 kati ya 40,695 waliofanya mtihani huo wamefaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu. Ufaulu huo ambao ni asilimia 96.97 umepanda kutoka asilimia 87.85 ya ufaulu wa wanafunzi waliofanya mtihani huo mwaka uliopita. Matokeo hayo yanaonyesha kwamba orodha ya shule kumi bora imetawaliwa na shule nyingi zenye majina yasiyo maarufu, fumbo ambalo tunadhani litahitaji kuteguliwa siyo tu na wanazuoni, bali pia na wasimamizi wa sera za elimu katika wizara husika.
Tunawapongeza wote waliohusika katika kuleta mafanikio hayo ya kihistoria, ikiwa ni pamoja na Necta yenyewe, kamati za uendeshaji mitihani za mikoa na wilaya, wakuu wa shule na wasimamizi wa mitihani hiyo kwa kuzingatia na kusimamia taratibu za uendeshaji mitihani, hivyo kuzuia vitendo vya udanganyifu vilivyokuwa vimetamalaki katika miaka ya nyuma. Kutokana na usimamizi huo mzuri, idadi ya wanafunzi waliogundulika wakifanya udanganyifu imezidi kupungua kutoka wanne mwaka uliopita hadi wawili mwaka huu. Hii inadhihirisha pasipo shaka kwamba watendaji katika wizara husika na taasisi zake wamejifunza kutokana na makosa ya huko nyuma. Tulizoea vitendo vya wizi wa mitihani, ucheleweshwaji wa vifaa, wasimamizi kutofika vituoni walikopangiwa na kadhalika.
Pamoja na ufaulu wa mwaka huu kuonekana kuchangiwa na idadi ndogo ya watahiniwa kulinganisha na mwaka uliopita, baadhi ya wachambuzi wamepinga matokeo hayo wakisema yametokana na hatua ya Serikali ya kushusha viwango vya ufaulu. Dhana inayotawala miongoni mwa wachambuzi hao ni kwamba matokeo hayo yanalenga kukidhi malengo ya kisiasa ili kuonyesha kwamba Mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), hususani katika sekta ya elimu umefanikiwa.
Hata hivyo, kinachowashangaza wengi ni matokeo hayo kuonyesha kwamba sekondari maarufu kama Tambaza na Iyunga ni miongoni mwa shule 10 zilizoshika mkia, huku Sekondari ya Kata ya Kisirimi iliyoko wilayani Arumeru, mkoani Arusha ikiibuka katika nafasi ya tatu kati ya shule 10 bora. Pia shule nyingi zilizokuwa zikitokea katika orodha ya 10 bora huko nyuma zimetupwa nje, huku ufaulu wa wanafunzi waliofanya mtihani wa Kiswahili ukiwa asilimia 99.98. Kama tulivyosema hapo juu, hali hiyo inahitaji tafsiri jadidi na mjadala mpana kitaifa.
Sisi hatuamini kwamba matokeo ya mtihani huo yamepindishwa. Hata hivyo, tunadhani kinachotakiwa sasa ni wizara husika kuhakikisha kwamba elimu inayotolewa inalenga kuwapa wanafunzi mbinu za kujitegemea badala ya nadharia. Pamoja na kuwapo umuhimu wa kupanua elimu, tunadhani pia wakati umefika wa kubadilisha mitalaa ili ijikite katika kutoa elimu ya kujitegemea. Mkazo uwekwe katika elimu ya ufundi, kwa maana ya kuhakikisha angalao kila wilaya inakuwa na chuo kimoja cha kutoa elimu stadi mfano wa VETA. Vinginevyo, majeshi tunayozalisha kila mwaka na kuyaweka vijiweni na mitaani yatasababisha maafa makubwa siku za usoni.
>>MWANANCHI
No comments