Breaking News

SHAHIDI WA KESI YA WIZI WA SIMU JNIA AELEZEA ILIVYOKUA

Dar es Salaam. Shahidi wa tatu katika kesi ya wizi wa simu zenye thamani ya Sh19 milioni, Koplo Frain amedai waliweka mtego uliofanikisha kuwakamatwa washtakiwa sita wakiwa na simu baada ya kuuziana.
Koplo Frain alieleza hayo jana wakati akitoa ushahidi katika Mahakama ya Wilaya Ilala, akiongozwa na Wakili Felista Mosha.
Alidai kuwa Januari 31, mwaka huu alipokea jalada la kesi ya wizi kutoka kwa mkuu wa upelelezi ambalo lilionyesha kuwa Januari 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J. Nyerere, watuhumiwa waliiba boksi moja lenye simu 460 za mkononi aina ya Techno na Itel zenye thamani ya Sh 19milioni.
Katika kesi hiyo inayowakabili wafanyakazi sita wa kampuni ya Swissport, washtakiwa hao wanadaiwa kuiba simu hizo mali ya Sued Chemchem. Koplo Frain alidai kuwa mzigo huo wa simu ulitokea China na ndege ya Shirika la Qatar, na kwamba baada ya kufanya uchunguzi waligundua kuwa simu hizo zilikuwa zinauzwa kariakoo kwa kijana mmoja.
Shahidi huyo aliendelea kuieleza mahakama kuwa baada ya kupata taarifa hizo, waliondoka na mlalamikaji pamoja na mpelelezi hadi katika Hoteli ya Valentino na kumkuta Mathias John aliyewahi kufikishwa mahakamani hapo lakini kwa sasa hayupo.
Koplo Frain alidai kuwa hotelini hapo, waliweka mtego ili waweze kumuuzia mlalamikaji simu na kufanikiwa kumkuta na simu 25 aina ya Itel zikiwa zimehifadhiwa katika  mfuko wa plastiki, alipoulizwa alidai kapewa na mfanyakazi wa kampuni ya Swissport aitwaye Hamisi Othuman.
Awali akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo, Wakili Mosha alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Januari 27, mwaka huu katika uwanja wa ndege. Wakili Mosha aliwataja washtakiwa hao  kuwa ni Hamad Mohamed(42), Haji Waziri (26), Yusuph Muhangwa (33), Hashimu Iddy(49), Ally Omary(33) na Hamis Othman (29).
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa siku hiyo washtakiwa kwa pamoja  waliiba boksi moja lenye simu 460 zikiwa na thamani ya Sh19milioni.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 19, mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa. Washtakiwa wote wako nje kwa dhamana.

No comments