Breaking News

WANAOMKOSOA JK HAWAKO SAHIHI

 
                                              Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salva Rweyemam
Ofisi ya Rais imesema kuwa wanaomkosoa Rais Jakaya Kikwete kuhusu msimamo wake katika mchakato wa Katiba Mpya hawako sahihi kwa kuwa ni mlezi na ana haki ya kutoa maoni yake kama mkuu wa nchi na kama mwanasiasa.
Pia, imewataka wasiokuwa wajumbe wa Bunge la Katiba waiache kazi hiyo mikononi mwa Bunge hilo kwa sasa hadi hapo rasimu itakapowasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya kuikubali au kuikataa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salva Rweyemamu ikiwa ni siku moja baada ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), kutoa tamko zito kwa Rais Jakaya Kikwete ikiishangaa kauli yake ya kupinga mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya Watanzania.
Rais Kikwete amekuwa akilaumiwa na taasisi na watu binafsi baada ya kulieleza Bunge la Katiba kuwa kuna baadhi ya mambo kwenye Rasimu ya Katiba ambayo hayawezekani kutekelezeka, akitoa mfano wa muundo wa Muungano wa serikali tatu, jambo ambalo CCT ilisema jana kuwa alitakiwa alifanye wakati Kamati ya Mabadiliko ya Katiba ilipokuwa ikimfuata kumweleza maendeleo ya kazi yao.
Hata hivyo jana, Rweyemamu aliliambia gazeti hili kuwa: “Kinachoendelea kwa sasa kwa baadhi ya makundi ya kidini kutoa matamko dhidi ya Rais si sahihi, kwa kuwa Rais ni mlezi na ana haki ya kutoa mtazamo wake kama mkuu wa nchi na kama mwanasiasa.”
Alisema kimsingi mchakato huo ni wa kisiasa na Rais ni mwanasiasa, pia ni mkuu wa nchi hivyo ndiye mwenye uwezo wa kutoa ushauri na kutoa angalizo pale inapohitajika, hasa anapoona kuna jambo lisilokuwa sawa, hivyo hakuna haja ya kuendelea kusimama kupinga kile alichokielekeza nje ya Bunge.
“Tulioko nje ya Bunge la Katiba hebu tuwaachie wajumbe. Rais kama msimamizi mkuu atakoseaje kwa kutoa ushauri? Alichokifanya ni sahihi na kama kuna tatizo, walioko nje ya Bunge warudi ndani ili wajadiliane kwa kina na kumaliza tatizo,” alisema.
Kauli ya CCM
Wakati Rweyemamu akisema kazi hiyo ya mjadala wa katiba iachwe kwa wajumbe wa chombo hicho cha kuandika Katiba, CCM ilisema jana kuwa kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake kuhusu mchakato huo na akaisifu CCT kwa kutumia haki hiyo ya kikatiba.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema katika mchakato wa kupatikana kwa katiba iliyo bora, kila mtu na kila kundi lina fursa ya kutumia uhuru wa kikatiba kueleza na kutoa maoni yao, hivyo viongozi hao wa CCT wametumia vyema uhuru huo.
Alisema kwamba anaamini CCT haikufanya hivyo kimakosa kama ambavyo makundi mengine, wakiwamo majaji, chama chake na hata watu binafsi wamekuwa wakifanya, kwa kutoa mitazamo yao kuhusu aina ya muundo wa Serikali wanayohitaji.
“Siyo hao tu, tunatarajia na wengine zaidi watatoa. Hiyo ni haki ya kimsingi iliyowekwa na Katiba. Hatupo hapa kwa ajili ya kushindanishwa, tunaamini Bunge lipo kwa mujibu wa sheria nalo litaendelea kusimamia taratibu zake, hatuna sababu ya kumziba mtu mdomo.”

No comments