Breaking News

DR.MANYAU NYAU MKOMBOZI WILAYA YA MKURANGA ASAMBAZA MRADI WA MAJI BURE

Mganga maarufu wa kienyeji, Dr. Manyaunyau ametoa msaada wa kusambaza maji bila kurudishiwa gharama yoyote kwa wakazi wa wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.

Akiongea na Sunrise ya 100.5 Times Fm, Dr Manyaunyau amesema ameanza kutoa huduma hiyo muda mrefu lakini hakujitokeza kwenye vyombo vya habari kueleza kwa kuwa nia yake haikuwa kujitangaza, hadi pale alipofuatwa na kipindi hicho na kuamua kuwaeleza watanzania.
Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Mercy Sila amethibitisha kuwa Manyaunyau amekuwa akitoa msaada huo na kwamba serikali kwa upande wake pia imekuwa ikiendelea na zoezi hilo kwa upande mwingine.
Nao wakazi wa Mkuranga wameelezea kuwa hivi sasa wanatumia zaidi maji yaliyosambazwa na Dr Manyaunyau kwa kuwa maji yanayosambazwa na halmashauri ya Mkuranga yamekuwa yakikatika kwa muda mrefu.
“Kwa kweli halmashauri ya Mkuranga tuna shida sana ya uhaba wa maji kutokana na kwamba tuna mabomba lakini mabomba mengi hayatoi maji. Maji yanayotumika sana ni ya Dr Manyaunyau, ambaye amesambazasambaza Mkuranga na watu wengi wameweka mabomba na wanapata maji majumbani mwao. Lakini kwa maji ya halmashauri, karibu miezi miwili mitatu maji hayatoki na yakitoka ni ya mgao. Yakitoka leo kesho hayatoki.” Amesema Mkazi wa Mkuranga.
Tovuti ya Times Fm ilizungumza na Dr Manyaunyau muda mfupi baadae na kikubwa tulitaka kufahamu gharama alizotumia kusambaza maji.
“Nilianza mdogomdogo lakini mpaka sasa hivi kwa tathimini ya haraka ya mradi wangu unafika mpaka kwenye 50 milioni, kwa kukadiriakadiria hivi inaweza kufika.” Amesema Manyaunyau.
Akieleza kuhusu idadi ya watu aliowasambazia maji katika wilaya hiyo, Manyaunyau ambaye mbali na kuwa mganga ni mfanyabiashara amesema yeye hufanya tu na hajakaa bado kuanza kuzihesabu kaya alizozihudumia.
Ameeleza kuwa lengo lake hasa ni kuhakikisha anaweza pia kuisaidia jamii kwa kiasi anachokipata kwa kuwa amejali kupata kutoka kwenye jamii hiyo hiyo.

No comments