Breaking News

GOLIKIPA WA COSTARICA ATUA REAL MADRID KWA MKATABA WA MIAKA 6

Navas: Mungu amesikia kilio changu cha muda mrefu
Mlinda mlango kutoka nchini Costa Rica, Keylor Antonio Navas Gamboa, amesema amefurahishwa na hatua ya kusajiliwa na klabu kubwa duniani ambayo alikuwa na ndoto za kuitumikia siku moja katika maisha yake.
Navas amesema anaamini dua na sala ambazo kila leo alikuwa akiomba kwa mungu wake, ndizo zimemfikisha hapo alipo na kilichobaki ni kujitahidi na kujiahakikishia nafasi katika ushindani wa kukaa langoni kwa msimu ujao wa ligi.
Amesema kitendo cha viongozi wa klabu ya Real Madrid kukubali kumsajili na kisha kumsainisha mkataba wa miaka sita, kinampa fikra za kujiamini na kutarajia makubwa kutoka kwenye klabu hiyo inayoushikilia ubingwa wa barani Ulaya kwa sasa.
"Mungu amesikia maombi yangu, amenisaidia na amenionyesha njia ya kufika nilipokuwa napahitaji kila siku, nitajitahidi kufanya kila niwezalo ili niendelee kuzisogelea ndoto za maisha yangu ya soka.”
"Mkataba wa miaka sita si haba, ni mkataba wa muda mrefu sana, unanipa mwanga na kuamini nitakuwa hapa kwa kipindi kirefu zaidi ambacho nitatakiwa kuonyesha ushupavu na ukamilifu wangu wote pale nitakapopata nafasi ya kuwa langoni mwa Real Madrid." Amesema Navas
Hata hivyo mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 27, amewataka mashabiki wake kuwa wastahamilivu katika kipindi hiki ambacho anatarajia kuwa katika hatua tofauti na alivyokuwa mwanzo.

No comments