Breaking News

BAADA YA MATOKEO MABOVU SIMBA FC YAJIPANGA USAJILI MPYA CHEKI HAPA KUJUA NI NANI NA NANI WAMETAJWA



Matokeo yasiyoridhisha ya Simba katika Ligi Kuu msimu huu yameufanya uongozi wa klabu hiyo uchanganyikiwe na kutaka kusajili kila mchezaji wamwonaye wakati huu wa usajili wa dirisha dogo.
Kutokana na presha hiyo, uongozi wa klabu hiyo umeshataja orodha ya wachezaji 11 ambao inataka kuwasajili kwa sasa ili kuimarisha kikosi.
Uongozi wa klabu hiyo unaonekana kuwataka wachezaji wengi kuliko timu zote zinazoshiriki  Ligi Kuu  na baadhi ya timu zimeonekana hazina mpango wa kuongeza wachezaji, nyingine zikitaka kuongeza wachache.
Alipoulizwa kuhusu usajili huo, katibu mkuu wa Simba, Stephen Ally alijibu:
“Kwanza, nani alisema tunawasajili wachezaji hao, hizo ni stori za vijiweni na za magazetini hivyo siwezi ku-comment (kusema lolote). “
Hata hivyo, uchunguzi wa  gazeti hili umebaini kuwa hadi sasa Simba imetangaza kuwataka wachezaji 11, idadi  ambayo ni sawa na kikosi kizima cha kwanza.
Wachezaji wanaohusishwa  na usajili mpya Simba ni kipa Juma Kaseja (Yanga), Said Morad (Azam), Emeh  Izuchukwu (Elverum Fc, Norway), Danny Mrwanda (Polisi Moro), Dan Sserunkuma (Gor Mahia, Kenya), Hamis Kessy, Salim Mbonde, Ame Ally (Mtibwa Sugar), Deus Kaseke (Mbeya City), Nurdin Chona na Salum Kimenya wa Prisons.
Kwa  maana hiyo, Simba inaweza kucheza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu kwa ufasaha ikiwa na wachezaji wapya zaidi ya waliocheza mechi saba na waliokuwapo huenda wakaishia benchi.
Kulingana na wachezaji hao kikosi cha kwanza Simba kinaweza kuwa:

Juma Kaseja, Salum Kimenya, Hamis Kessy, Said Morad, Salim Mbonde, Nurdin Chona, Dan Sserunkuma, Deus Kaseke, Ame Ally, Danny Mrwanda,  Emeh Izuchukwu. Hata hivyo  kuna baadhi ya wachezaji  itakuwa vigumu kwa Simba kuwanasa  msimu huu.
Miongoni mwao ni Izuchukwu, raia wa Nigeria anayesemekana anapigiwa chapuo na kigogo mmoja wa timu hiyo, lakini baadhi ya viongozi hawakubalini na hilo.
Beki Morad anatakiwa  abadilishane na kiungo Amri Kiemba kwenda Azam, ndipo aachiwe atue Msimbazi.
Mganda Sserunkuma atasajiliwa kuziba nafasi ya Pierre Kwizera au Raphael Kiongera, ambao wanatarajiwa kuachwa, ingawa jambo hilo  litakuwa gumu kwani itategemea makubaliano baina ya pande mbili, yaani mchezaji na uongozi  wa Simba.
Hata hivyo, endapo mchezaji atagoma kuachwa au kutolewa kwa mkopo, Simba itabidi itafute njia nyingine kwani  kanuni za usajili wa dirisha dogo haziruhusu kuachwa mchezaji, isipokuwa kwa makubaliano maalumu.

Pia, klabu hiyo inaweza kupata wakati mgumu kumpata Mrwanda aliyesaini mkataba wa muda mfupi na Polisi Morogoro aliyoichezea mechi saba na sasa anataka kurejea Vietnam kucheza soka la kulipwa.
 Wachezaji wengine wote Simba inaweza kuwapata kirahisi kama ikikubaliana na klabu wanazotoka na tayari imeshawaleta Dar es Salaam  Kaseke, Chona na Kimenya kwa ajili ya mazungumzo ya awali.

No comments